Ukosefu wa vyumba vya madarasa wasababisha wanafunzi wilayani Meatu kusomea chini ya Mbuyu.
Wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi zilizopo katika kata ya Mwangudo wilayani Meatu mkoani Simiyu wanasomea chini ya miti ikiwemo mibuyu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Shule hizo ikiwemo shule ya msingi Mbuyuni na Ng’ungulu zenye idadi ya wanafunzi wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 600 kila moja ina vyumba viwili tu vya madarasa, matundu mawili ya vyoo na walimu wawili, mmoja ni mwajiriwa wa serikali na mwingine ni mwalimu wa kujitolea ambapo mwalimu wa zamu wa shule ya msingi Mbuyuni Emmanuel Robert ameiambia ITV kuwa uhaba wa madarasa ni changamoto inayohitaji ufumbuzi wa haraka.
Akizungumzia kuhusu changamoto hizo, kaimu mkurugenzi wa mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu Pamba Hezron amewahimiza wananchi na viongozi wa vijiji kujenga vyumba vya madarasa na nyumba za walimu huku akiahidi halmashauri kushughulikia tatizo la walimu na vifaa vya kufundishia.
Nae meneja uhifadhi na maendeleo ya jamii wa makampuni ya kitalii ya Mwiba holdings na TGTS Batro Ngilangwa amesema uhaba wa miundombinu ya elimu katika shule zinazopakana na mapori ya akiba ya maswa na jumuiya ya wanyamapori ya makao umezigusa taasisi hizo ambazo zimechangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati.
Comments
Post a Comment