Waziri Mkuu Ataka Mkataba Uvunjwe....Ni wa Mkandarasi aliyenyang’anywa pasipoti na Rais Magufuli
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo na ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda uliopangwa. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, jana (Alhamisi, Machi 30, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la mto Wami, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani. Alikuwa ameenda kukagua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza majisafi pamoja na matenki ya kuhifadhia maji ambao umechukua muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu ya kwanza ilianza mwaka Septemba mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003. Alimuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ahakikishe kuwa kazi ya ujenzi wa mradi huo inaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo, wakamilishe taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine. Agizo la Waziri Mkuu linafuatia taarifa aliyopewa kw...